Friday 14th, November 2025
@SHULE YA SEKONDARI YA KUTWA LIWALE NA SHULE YA SEKONDARI YA KIBUTUKA

Wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa vituo vya kupigia kura katika Jimbo la Liwale wameanza mafunzo maalum leo mara baada ya kula kiapo cha maadili kinachowataka kutunza siri za mchakato wa uchaguzi na kutokuwa wanachama wa chama chochote cha siasa wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.
Mafunzo hayo yatakayodumu kwa siku mbili (leo na kesho) ni sehemu ya maandalizi ya mwisho kuelekea uchaguzi mkuu, yakifuata mafunzo ya awali yaliyotolewa jana kwa makarani waongoza vituo ambayo yalikuwa ya siku moja.
Akifungua mafunzo hayo, Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Liwale, Bw. Winfrid Tamba, aliwataka washiriki kuzingatia maadili, uwajibikaji na weledi wakati wote wa usimamizi wa vituo vya kupigia kura.
Aidha, amewasisitiza wasimamizi kuzingatia taratibu za uendeshaji wa vituo ikiwemo muda sahihi wa ufunguzi na ufungaji wa vituo, pamoja na namna ya kushughulikia wapiga kura kwa kuzingatia kanuni, haki na usawa. Pia wametakiwa kutoa kipaumbele kwa makundi maalum kama wazee, watu wenye ulemavu, wagonjwa na wanawake wajawazito ili wasilazimike kusubiri kwa muda mrefu kwenye foleni.
Mafunzo hayo yanafanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Liwale (Liwale Day) na Shule ya Sekondari Kibutuka, huku yakielezwa kuwa ni hatua muhimu ya kuimarisha maandalizi ya mwisho kuelekea siku ya kupiga kura itakayofanyika Jumatano wiki ijayo, Oktoba 29, 2025.
Along Nachingwea Road opposite DDD Quarters
Sanduku la Posta: P.O. BOX 23 LIWALE
Simu ya Mezani: 023 2937043
Mawasiliano ya mkononi:
Baruapepe: ded@liwaledc.go.tz
Hakimiliki 2023 © Halmashauri ya Wilaya ya Liwale. Haki zote zimehifadhiwa.