Mkuu wa Wilaya ya Liwale, Mheshimiwa Goodluck Mlinga, amefanya ziara ya ukaguzi katika vitalu viwili vya uchenjuaji wa madini ya dhahabu vilivyopo chini ya wawekezaji Ezekiel Mohamed Hamis na Kampuni ya Uchimbaji Madini ya JIAPA (JIAPA Gold Mining) katika Kijiji cha Lilombe, Jumanne, Disemba 2, 2025.
Katika ziara hiyo, Mlinga amesisitiza umuhimu wa kuzingatia taratibu zote za utunzaji wa mazingira, hususan udhibiti wa maji yenye kemikali aina ya molecule yanayotumika katika uchakataji wa dhahabu. Amesema ni lazima kuhakikisha maji hayo hayaingii kwenye mito inayotegemewa na wananchi kwa matumizi ya kila siku, ili kulinda afya za jamii pamoja na mazingira ya eneo hilo.
Aidha, DC Mlinga amewataka wawekezaji kuhakikisha mazingira ya migodi yao yanawekwa katika hali salama kabla ya kuanza kwa msimu wa mvua. Amesema mvua zinaweza kusababisha mifumo ya maji kujaa na hatimaye kuruhusu maji yenye kemikali kuingia kwenye mikondo ya maji ya asili, jambo linaloweza kuleta athari kubwa kwa wananchi wanaotumia maji ya mito hiyo.
Amesisitiza wajibu wa kuwa na mpango mkakati madhubuti wa kudhibiti maji taka yanayotokana na shughuli za uchenjuaji. Amesema mpango huo ni lazima uonyeshe hatua za haraka na za muda mrefu za kuzuia uchafuzi wa mazingira na kulinda usalama wa vyanzo vya maji.
Katika ziara hiyo iliyolenga kufahamu mwenendo wa shughuli za uchakataji wa madini pamoja na tathmini ya hatua za kimazingira zinazochukuliwa na wawekezaji hao, Mheshimiwa Mlinga aliambatana na Katibu Tawala wa Wilaya, Bi. Azilongwa Bohari, pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya (KUU).
Along Nachingwea Road opposite DDD Quarters
Sanduku la Posta: P.O. BOX 23 LIWALE
Simu ya Mezani: 023 2937043
Mawasiliano ya mkononi:
Baruapepe: ded@liwaledc.go.tz
Hakimiliki 2023 © Halmashauri ya Wilaya ya Liwale. Haki zote zimehifadhiwa.