Halmashauri ya Wilaya ya Liwale imeendelea kutekeleza agizo la Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan linalotaka Halmashauri kutoa mikopo ya asilimia 10 kwa wanawake, vijana na walemavu ambapo leo Juni 8, 2025 Halmashauri ya Wilaya ya Liwale imetoa mkopo wa shilingi milioni 605,006,870 kwa vikundi 161 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Akisoma taarifa kwa mgeni rasmi Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Ndg. Hamisi Namaleche amesema kuwa hadi kufikia Mei 30, 2025 Halmashauri ya Wilaya ya Liwale imefanikiwa kutoa mikopo yenye Jumla ya shilingi milioni 773,523,370 kwa vikundi 201 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ambapo mikopo hiyo imetolewa kwa awamu mbili.
Ameendelea kufafanua kuwa katika awamu hizo mbili, awamu ya kwanza Halmashauri imetoa mkopo wenye jumla ya shilingi milioni 168,516,500 na awamu ya pili Halmashauri imetoa mkopo wenye thamani ya shilingi milioni 605,006,870 na kufanya jumla ya shilingi milioni 773,523,370.
Mkopo huu wa awamu ya pili wenye thamani ya shilingi 605,006,870 umetolewa kwa vikundi 161 ambapo vikundi 10 ni vya walemavu, vikundi 53 vijana na vikundi 98 ni wanawake.
Namaleche amesema kuwa lengo la kutoa mkopo huo ni kuongeza ajira na kuimarisha uchumi wa vijana.
Katika hafla hiyo iliyofanyika kwenye viwanja vya Reiners Mgeni rasmi ambaye ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Liwale Mhe. Mohamed Mtesa amekabidhi pikipiki 11 na maguta 11 kwa vikundi 9 vya vijana wanaojihusisha na biashara ya usafirishaji ambao ni miongoni mwa wanufaika wa mikopo ya awamu ya pili kutoka Halmashauri.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Liwale Mhe. Mohamed Mtesa amevitaka vikundi 161 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu vilivyopata mikopo ya asilimia 10 awamu ya pili wenye thamani ya shilingi milioni 605,006,870 kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Liwale kufanya marejesho kwa wakati ili kuepuka usumbufu.
''Mliokopeshwa hakikisheni mnafanya marejesho na yaende kwa wakati, ikitokea kama kuna wiki utashindwa kurejesha toa maelezo mapema, tukiyafanya haya inatupa nafasi kubwa ya kukukopesha zaidi ya kile tulichokupa mwanzo'' amesema Mhe. Mtesa
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Liwale Bi. Tina Sekambo amewaasa wanufaika wa mikopo ya asilimia 10 iliyotolewa na Halmashauri kutafuta maeneo yenye masoko kwa ajili ya biashara zao ili kuepuka msongamano.
Bi. Sekambo amesema kuwa kama wanufaika hao wa mikopo wanaona msongamano wa biashara ni mkubwa Mjini hawazuiliwi kutafuta masoko sehemu nyingine ili waweze kufanya marejesho ya fedha hizo.
Aidha Sekambo amewataka vijana waliokopeshwa vifaa vya usafiishaji kutunza vifaa hivyo ili viweze kudumu na kuwasaidia kufanya marejesho kwa wakati pia amewasisitiza waliopewa mikopo ya fedha kuepuka migogoro katika vikundi vyao.
Hayo yamesemwa Juni 8, 2025 katika hafla ya kukabidhi mkopo wenye thamani ya shilingi milioni 605,006,870 kwa vikundi 161 vya wanawake, vijana na walemavu iliyofanyika katika viwanja vya Reiners Liwale Mjini.
Vikundi vya Usafirishaji vilivyopata Mkopo ni Transporters kilichopo kata ya Likongowele,kimepokea Guta tano(05),Bodaboda Mbonde kilichopo kata ya Nangando kimepokea Pikipiki tano(05),Umoja ni Ushindi kilichopo kata ya Kichonda kimepokea Guta mbili(02),Tumaini Mkonganage kilichopo kata ya Mangirikiti kimepokea pikipiki tatu(03),Kipule One kilichopo kata ya Mangirikiti kimepokea pikipiki mbili(02),Ukombozi kilichopo kata ya Mkutano kimepokea Guta Moja(01),Mama Samia kilichopo kata ya Mpigamiti kimepokea Guta Moja(01),Sinza Vijana kilichopo kata ya Mbaya kimepokea Guta Moja(01),Mshikamano kilichopo kata ya Kimambi kimepokea Guta moja(01),Vijana Maendeleo kilichopo kata ya Ngongowele kimepokea Pikipiki moja(01).
Along Nachingwea Road opposite DDD Quarters
Sanduku la Posta: P.O. BOX 23 LIWALE
Simu ya Mezani: 023 2937043
Mawasiliano ya mkononi:
Baruapepe: ded@liwaledc.go.tz
Hakimiliki 2023 © Halmashauri ya Wilaya ya Liwale. Haki zote zimehifadhiwa.