Katibu Tawala wa Wilaya ya Liwale, Bi. Azilongwa Bohari, amesema serikali imejipanga kuboresha uchumi wa wakulima wa korosho kwa kuhakikisha sio tu wanazalisha, bali pia wanapata fursa za kufikia masoko ya moja kwa moja hadi kwa watumiaji wa mwisho.
Amesema hatua hiyo, ikichangiwa na mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya halmashauri, itawasaidia wakulima na vikundi vya ubanguaji kuongeza thamani ya korosho na kukuza kipato chao.
Bi. Bohari ameyasema hayo wakati wa Kongamano la Fursa za Mitaji, Teknolojia na Masoko kwa Vikundi vya Ubanguaji wa Korosho Wilaya ya Liwale, lililoandaliwa na Benki ya NMB kupitia NMB Foundation. Kongamano hilo liliwakutanisha viongozi wa serikali, taasisi za fedha, wadau wa sekta ya korosho, na teknolojia.
Katika kongamano hilo, Bohari alitembelea maonyesho ya mitambo ya kisasa ya ubanguaji wa korosho isiyotumia umeme na inayotumia umeme na mafuta, na kusema teknolojia hizo zitawawezesha wakulima kuongeza ufanisi, kuboresha ubora wa bidhaa na kuongeza thamani ya korosho katika soko.
Kwa upande wake, Meneja wa Benki ya NMB Tawi la Liwale, Marystella Kalimasi, amesema kupitia NMB Foundation, benki hiyo imeweka mkakati wa kuongeza mikopo kwa wakulima na vikundi vya ubanguaji wa korosho ili kuimarisha uzalishaji na kuongeza tija. Amesema mikopo hiyo inalenga kuongeza mtaji wa uzalishaji na kuwawezesha wakulima kushindana kwenye masoko yenye mahitaji makubwa.
Kalimasi amesema NMB pia inatoa mikopo ya ununuzi wa mashine za kisasa za ubanguaji wa korosho kupitia ushirikiano na watengenezaji na wasambazaji wa mitambo hiyo. Amesema hatua hiyo inalenga kupunguza gharama za uzalishaji na kuwawezesha wanavikundi kuzalisha kwa viwango vinavyokubalika kitaifa na kimataifa.
Along Nachingwea Road opposite DDD Quarters
Sanduku la Posta: P.O. BOX 23 LIWALE
Simu ya Mezani: 023 2937043
Mawasiliano ya mkononi:
Baruapepe: ded@liwaledc.go.tz
Hakimiliki 2023 © Halmashauri ya Wilaya ya Liwale. Haki zote zimehifadhiwa.