Mkuu wa Wilaya ya Liwale Mheshimiwa Goodluck Mlinga amepokea taarifa ya tathmini ya elimu na ugawaji wa tuzo za ufaulu katika matokeo ya mitihani ya Kitaifa ya kidato cha nne, kidato cha sita, na darasa la saba mwaka 2023 kwenye ukumbi wa shule ya sekondari Liwale Day.
Wilaya ya Liwale ina jumla ya shule za msingi 65, kati ya hizo shule 64 ni za umma na 1 ni ya binafsi. Wilaya ina shule za Sekondari 19 na shule zote ni za umma. Wilaya ina vituo 3 vya Walimu (TRC) na kituo 1 cha Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima.
Wilaya ya Liwale imekuwa na utaratibu wa kuendesha mitihani na upimaji wa kitaifa ili kuweza kuwandaa wanafunzi wetu vizuri katika kushindana na kuongeza ufaulu katika shule zetu jambo ambalo limepelekea wilaya kufanya vizuri katika madarasa yote ya mitihani iliyofanyika mwaka huu 2023.
Katika mpango wa mwaka 2023, wilaya ililenga kuongeza ufaulu kwa madarasa yote ya mitihani kwa 100% kwa darasa la Nne, 90% kwa Darasa la saba, 100% kwa kidato cha Pili 100% kwa kidato cha Nne na 100% kwa kidato cha sita, Katika Matokeo ya Mitihani wa kidato cha sita iliyotangazwa Mwezi Julai 2023, wilaya imefikia lengo la kufaulisha wanafunzi wa kidato cha sita kwa 100% na kuendelea. Aidha, Matokeo ya kumaliza Elimu ya Msingi ya mwaka 2023 yanaonesha kuwa, wilaya yetu imepata ufaulu wa 92.01% kutoka 90.27% mwaka 2022 hii ikiwa ni ongezeko la 1.74% na hivyo kufanya wilaya ya liwale kushika nafasi ya pili katika Mkoa wa Lindi.
Katika utoaji wa tuzo hizo Mheshimiwa Mlinga amewapongeza wanafunzi wote walio fanya vizuri na walimu wao ambao wamepokea tuzo kwa kufanya vizuri katika masomo yao na kufundisha na pia amewataka walimu kuendelea kufanya kazi kwa bidii na walimu ambao wanafundisha maeneo yenye mazingira magumu waweze pia kupewa tuzo ili ziweze kuongeza motisha kwa walimu hawa, napia amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri kuhakikisha anawalipa walimu wote ambao wanadai madai yao ili kuondoa malalamiko, na mwakani tuzo hizi ziweze kuboreshwa zaidi na kuongeza vipengele ambavyo vimependekezwa na wajumbe.
Pia ametoa wito kwa walimu wote kuhakikisha wanakuwa waadilifu kwa kuwafundisha watoto wetu na kuwalea vizuri huko mashuleni kwani kumekuwa na walimu wachache ambao wanafanya vitendo vya kihovu ikiwa ni kutembea na wanafunzi hivyo waache mara moja na ambaye atabainika basi sheria itachukua mkondo wake na hivyo walimu na wanafunzi tunawajibu wa kushirikiana ili tuweze kufanya vizuri zaidi.
Aidha Mheshimiwa Mlinga ametoa maagizo kwa Maafisa elimu wote wa Kata zote kuhakikisha wanapeleka idadi ya watoto na majina yao ambayo wanafunzi hawajaenda shule na kuacha shule kwenye ofisi yake ili aweze kuwafatilia na kuwakamata na kuwapeleka Mahakamani pamoja na wazazi wao pia ametoa wito kwa vingozi mbalimbali ikiwemo Madiwani na viongozi wa vijiji kuhakikisha wanasimamia masuala ya elimu kwenye Kata zao na kutunza mindombinu ya madarasa na pia vijiji vyote vyenye mapato yatokanayo na misitu kuhakikisha vinachangia kwenye shule ili wanafunzi waweze kupata chakula wakiwa shuleni hii itasaidia kupunguza utoro na kuongeza ufaulu .
Aidha Mheshimiwa Mlinga amesema changamoto zote ambazo zimeelezwa serikali imezibeba na kwenda kuzifanyia kazi lengo likiwa ni kuboresha mazingira ya ufundishaji lakini pia tunaipongeza serikali ya awamu ya sita kwa kazi kubwa na nzuri inayofanya katika kuboresha miundombinu ya shule ambayo imesaidia sana kuyafikia mafaniko haya ndani ya Wilaya hii ya Liwale na pia tuendelee kushirikiana ili tuweze kusonga mbele zaidi.
Picha mbalimbali katika zoezi la ugawaji wa Tuzoa za walimu na wanafunzi walio fanya vizuri kwa mwaka 2023 katika madarasa ya mitihani.
Along Nachingwea Road opposite DDD Quarters
Sanduku la Posta: P.O. BOX 23 LIWALE
Simu ya Mezani: 023 2937043
Mawasiliano ya mkononi:
Baruapepe: ded@liwaledc.go.tz
Hakimiliki 2023 © Halmashauri ya Wilaya ya Liwale. Haki zote zimehifadhiwa.