Taasisi isiyo ya kiserikali ya WAJIBU kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) na Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), imeendesha mafunzo kwa makundi maalumu katika Halmashauri ya Wilaya ya Liwale, mkoani Lindi.
Mafunzo hayo yamelenga kuwawezesha washiriki kufahamu Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2023 na kanuni zake, ambazo zinaelekeza taasisi za ununuzi kutenga asilimia 30 ya bajeti ya mwaka kwa ajili ya makundi maalumu kushiriki katika zabuni za umma. Makundi hayo ni wanawake, vijana, wazee na watu wenye ulemavu.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Afisa Ununuzi kutoka TAMISEMI, Bw. Amiri Mhando, aliwahimiza washiriki kutumia ipasavyo fursa zilizopo, ikiwemo mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri. Aliongeza kuwa, TAMISEMI imeanza mchakato wa kutafuta uwezekano wa taasisi za umma kutoa kianzio cha kazi (advance payment) kwa makundi yatakayopata zabuni, ambacho kitarejeshwa baada ya mauzo.
Kwa upande wake, Afisa Ununuzi kutoka PPRA, Bi. Tumpe Ngalla, alisema mpango huo unalenga kutoa fursa sawa kwa makundi maalumu kushiriki katika biashara za serikali na kuchangia ukuaji wa uchumi wa wananchi. Naye Afisa Tehama wa PPRA, Bw. Damas Makweba, aliwahimiza washiriki kuhakikisha wanajisajili rasmi katika mfumo wa NeST ili kushindania zabuni zinazotolewa na taasisi za umma.
Afisa Ufuatiliaji na Tathmini kutoka WAJIBU, Bi. Tekla Mleleu, alishukuru mwamko wa makundi maalumu kushiriki mafunzo hayo na kubainisha kuwa WAJIBU ni taasisi isiyo ya kiserikali yenye lengo la kuinua jamii kupitia kukuza uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa fedha za umma.
Aidha, alifafanua kuwa kupitia ufadhili wa Balozi za Norway na Sweden, WAJIBU imeshirikiana na PPRA pamoja na Ofisi ya Rais – TAMISEMI kuwezesha mafunzo hayo kwa makundi maalumu, huku akiwahimiza washiriki kutumia ipasavyo fursa hiyo kujifunza mfumo wa NeST na namna ya kushiriki katika zabuni za umma kupitia wakufunzi wa PPRA na OR-TAMISEMI.
Along Nachingwea Road opposite DDD Quarters
Sanduku la Posta: P.O. BOX 23 LIWALE
Simu ya Mezani: 023 2937043
Mawasiliano ya mkononi:
Baruapepe: ded@liwaledc.go.tz
Hakimiliki 2023 © Halmashauri ya Wilaya ya Liwale. Haki zote zimehifadhiwa.